Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazoezi ya yoga ni sambamba na maadili ya Umoja wa Mataifa

Mazoezi ya yoga ni sambamba na maadili ya Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kwamba Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeamua kuadhimisha siku ya kimataifa ya yoga, tarehe 21, Juni, kwani ni aina ya mazoezi au masomo ambayo maadili yake ni sambamba na yale ya Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Ban amenukuliwa akisema kwamba mazoezi hayo yanayochezwa tangu enzi za kale yana manufaa kwa afya ya mwili na akili ya binadamu, na pia yanaweza kuimarisha maisha ya watu kwa ujumla.

Aidha Bwana Ban amesema kila mtu anaweza kufanya mazoezi ya yoga, na kwamba masomo hayo yanakuza heshima kwa binadamu na mazingira tunapoishi, akiongeza kwamba yeye mwenyewe ni shahidi kwa kuwa amejaribu yoga alipotembelea nchini India mwaka 2014.

Akihojiwa na Redio ya Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Kudumu wa India kwenye Umoja wa Mataifa, Asoke Mukerji, amesema kwamba yoga inapendwa sana na watu duniani kote siku hizi, wakati ambapo watu wanakumbwa na msongo na shinikizo la kifikra.

“ Ni njia mbadala ya kukabiliana na shinikizo la maisha ya kila siku, na kwa sababu inaweza kuondoa msongo wa binadamu na kumwezesha kumakinika, ndio inapendwa sana, pia haigharimu chochote, unaweza kufanya yoga kwenye sehemu yoyote, na blanketi au godoro tu.”