Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya amani ya Yemen yamalizika, matumaini yapo

Mazungumzo ya amani ya Yemen yamalizika, matumaini yapo

Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed amesema kufanyika kwa mazungumzo na pande zote za mzozo mjini Geneva Uswisi nimafanikio makubwa.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Geneva, Bwana Ould Cheikh Ahmed amesema ingawa mwafaka haukupatikana, msingi wa kuafikiana sitisho la mapigano upo na sasa ni lazima kuendelea na mazungumzo, licha ya changamoto na matatizo.

(SAUTI AHMED)

“ Tunapaswa kutambua sisi sote kwamba mazungumzo ya Geneva si mwisho, lakini ni mwanzo wa safari ndefu na ngumu, iliyoandaliwa na mazungumzo ya awali na wayemeni. Mlango umefunguliwa kwa Wayemeni kuendelea na mazungumzo.”

Aidha amemulika hali mbaya ya kibinadamu akikariri wito wa Katibu Mkuu wa kusitisha mapigano kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu wakati wa mwezi wa Ramadan.

Mjumbe maalum amesema anaelekea New York kuripoti mbele ya Baraza la Usalama kuhusu mazungumzo hayo.