Wataalam wa UM walaani mauaji ya Wamarekani wenye asili ya Afrika
Wataalam wa Jopo la Umoja wa Mataifa la linalohusika na masuala ya watu wenye asili ya Afrika, wamelaani vikali shambulio dhidi ya kanisa la Emanuel African Methodist katika mji wa Charlston, jimbo la South Carolina wiki hii, na ambalo liliwaua watu tisa raia wa Marekani wenye asili ya Afrika.
Katika taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa jopo hilo, Bi Mireille Fanon Mendes-France, wataalam hao wamekaribisha hatua za haraka zilizochukuliwa na mamlaka kuchunguza kitendo hicho cha uhalifu wa chuki kwa misingi ya rangi.
Amesema juhudi zote zinapaswa kufanywa ili kuhakikisha kuwa mtu aliyetekeleza mauaji hayo anashtakiwa na kupewa adhabu inayostahili.
Wataalam hao wamesema hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kuzuia matumizi katili ya bunduki, na uhalifu wa unaotokana na chuki za rangi, ambao unaathiri usalama wa Wamarekani wenye asili ya Afrika, jamii zao na dunia kwa ujumla.