Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangura apongeza kuifanya Juni 19 Siku ya Kupinga ukatili wa kingono vitani

Bangura apongeza kuifanya Juni 19 Siku ya Kupinga ukatili wa kingono vitani

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika migogoro, Zainab Hawa Bangura, amezipongeza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, hususan serikali ya Argentina, kwa kwa kuendelea kulipa kipaumbele suala la ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, na kupitisha azimio la kuitangaza Juni 19 kama Siku ya Kimataifa ya kupinga ukatili wa kingono katika maeneo yenye migogoro.

Bi Bangura pia ameshukuru wale wote wanaohatarisha maisha yao wakijaribu kulitokomeza janga hilo. Amesema siku hii maalum inaongeza msukumo wa kuwataja na kuwaenzi maelfu ya manusura wa ukatili wa kingono, wakiwemo wanawake, wasichana, wanaume na wavulana, ambao licha ya madhara waliyopata, wameonyesha ari na ujasiri usiolegea, ili kulizungumzia janga hili.

Amesema, miaka saba ilyopita, azimio namba 1820 lilipishwa likitambuwa kwa mara ya kwanza kuwa suala la ukatili wa kingono na suala la amani na usalama, na ambalo linahitaji kukabiliwa kiusalama, kisheria na kwa huduma.

“Tangu wakati huo, tumeshuhudia msukumo wa kisiasa wa aina yake. Changamoto tuliyo nayo sasa kugeuza utashi huo wa kisiasa kuwa vitendo na ulinzi panapotakiwa. Maadhimisho haya ya kila mwaka yatakuwa kama mbiu ya kuchukua hatua.”

Bi Bangura amesema kuwa janga la ukatili wa kingono hugusa kila sehemu ya dunia, akitoa mfano way ale aliyojionea hivi karibuni alipozuru Mashariki ya Kati, na zamani kwingineko.