Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya dola milioni 20 zahitajika kuwasaidia wakulima wa Nepal

Zaidi ya dola milioni 20 zahitajika kuwasaidia wakulima wa Nepal

Shirika la Kilimo na Chakula Duniani(FAO) limesema kwamba wakulima wa Nepal wanahitaji dola milioni 20 kwa ajili ya kuwawezesha kurejelea shughuli za kilimo ili kukabiliana na ukosefu wa uhakika wa chakula unaoshuhudiwa miongoni mwa watu milioni moja nchini humo.

Kulingana na FAO, ni asilimia 13 tu ya ombi la dola milioni 23.4 ya ufadhili wa kilimo wa dharura imepatikana.

Matetemeko mawili ya ardhi yalitokea mwezi Aprili na Mei mwaka huu, yakisababisha vifo vya watu zaidi ya 8,000, huku yakisambaratisha maeneo mengi nchini Nepal.

Aidha janga hilo limesamabaratisha pia shughuli za kilimo huku likihatarisha vipato vya familia za vijijini.

Kulingana na utafiti uliongozwa na FAO, katika wilaya sita Nepal ambazo ziliathirika pakubwa, nusu ya kaya zilipoteza mazao yao ikiwemo mchele, mahindi, ngano na mpunga.

Kadhalika matetemeko hayo yaliharibu vifaa vya kilimo, mashamba na pembejeo.