Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatoa wito kwa Jamhuri ya Dominika kutofukuza raia wasio na utaifa

UNHCR yatoa wito kwa Jamhuri ya Dominika kutofukuza raia wasio na utaifa

Shirika la Umoja  wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limetoa wito leo kwa Jamhuri ya Dominika kutofukuza watu ambao uraia wao umekuwa mashakani tangu uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba ya mwaka 2013. Taarifa zaidi na Grace Kaneyia. (Taarifa ya Grace)

Msemaji wa UNHCR Adrian Edwards amewaambia leo waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kwamba zaidi ya watu 200,000 wanakadiriwa kutokwua na uraia nchini Jamhuri ya Dominika, watu hao wakiwa wenye asili ya Haiti waliozaliwa nchini humo.

Ameongeza kwamba uamuzi wa mahakama uliowapa hadi katikati mwa mwezi Juni kujisajili, unaweza kuathiri maelfu ya watu:

"Hii italeta madhara makubwa kwa waathirika na itakuwa kikwazo kikubwa katika juhudi za kimataifa za kumaliza tatizo la kukosa utaifa. Ni muhimu sana kwamba Jamhuri ya Dominika  ichukue hatua muhimu ili kuzuia kufukuzwa kwa mtu yeyote wa Dominika asiyekuwa na utaifa na hatma yake ukizingatia haki za binadamu, na kuepuka kuweka mazingira yatakayosababisha ukimbizi"