Serikali zina haki ya kunikosoa: Zerrougui

Serikali zina haki ya kunikosoa: Zerrougui

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na mizozo, Leila Zerrougui amesema kitendo cha baadhi ya nchi kukosoa ripoti ya hivi karibuni kuhusu hali ya watoto kwenye mizozo, ni dalili kuwa wanafanya kazi yao vizuri.

Bi. Zerrougui amesema hayo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari mjini New York, Marekani baada ya kuhutubia Baraza la Usalama kwenye mjadala wa watoto na mizozo.

Ripoti hiyo imetaja madhila wanayopata watoto kwenye mizozo ikiwemo huko Ukanda wa Gaza ambapo mwandishi mmoja alihoji anapokea vipi shutuma kutoka baadhi ya serikali zilizotajwa kwenye ripoti hiyo.

(Sauti ya Leila)

“Sina tatizo na kile ambacho serikali zinasema kwa kuwa ni haki yao. Lakini ninachotaka kusisitiza ni kwamba hakuna jambo jipya tulilobuni mwaka huu. Ni mchakato ule ule tuliotumia kwa kila serikali, tangu hizi serikali zianze kuwepo katika ripoti hii. Israel katika ripoti hii tangu mwaka 2005. Kila mwaka mchakato ni ule ule kanuni ni zile zile, mwaka jana nilikuwepo hapa sikulaumiwa kwa kukiuka taratibu, halikadhalika mwaka uliotangulia.”

Akaenda mbali zaidi kuelezea mchakato ulioptiwa..

(Sauti ya Leila-2)

 “Japokuwa mwaka huu kwa kuwa tulifahamu kuwa muda ni mdogo na lazima tuwasilishe ripoti mwezi Juni badala ya mwezi Septemba tuliwapatia muda zaidi , tuliwapatia wiki mbili ambazo tunazipatia serikali, waliomba muda zaidi tukawapa siku tatu, walitupatia maoni yao, tunajumuisha kile ambacho kinafaa, serikali zinatupatia maoni yao, hatuwezi kuweka maoni  ya kila mtu, tunaweka kweneye kitabu. Kwa hiyo hicho ndio tunafanya na serikali zina haki ya kutukosoa na sina tatizo na hilo.

Mapema akihutubia baraza la usalama Bi. Zerrougui amesisitiza umuhimu wa pande zote kwenye mzozo iwe serikali au vikundi visivyo vya kiserikali kuchukua hatua kulinda watoto kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na ukwepaji wa sheria udhibitiwe.