Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Karibu majimbo yote ya Yemen yamekumbwa na mzozo wa chakula

Karibu majimbo yote ya Yemen yamekumbwa na mzozo wa chakula

Hali ya uhakika wa chakula nchini Yemen inazidi kuzorota, huku majimbo 19 kati ya 22 yakiorodhesha kwenye hali ya mzozo au dharura, imesema taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Chakula na Kilimo FAO, lile la Mpango wa Chakula Duniani WFP na serikali ya Yemen.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, idadi ya watu wanaokumbwa na ukosefu wa uhakika wa chakula nchini humo imeongezeka kwa asilimia 17 tangu mapigano yalipoongezeka mwisho wa mwezi Machi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini New York, Marekani, Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema sasa watu wapatao milioni 13 hawana chakula cha kutosha nchini Yemen.

“ Kiwango cha utapiamlo wa kupindukia kimeongezeka pia, watu wengi wakilazimika kula mara chache zaidi kwa siku au kula vyakula venye bei nafuu zaidi  na vinavyorutubisha kidogo zaidi. Mzozo, ukosefu wa usalama na upungufu wa mafuta vimesababisha bei kupanda, mbali na kuhatarisha zaidi familia ambazo tayari zinateseka”

Aidha Bwana Haq amesema, Yemen inahitaji sitisho la mapigano, ufadhili na usafirishaji bora kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu na kurejeshwa kwa biashara ya bidhaa kutoka nje.