Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama launga mkono makubaliano ya amani Mali

Baraza la Usalama launga mkono makubaliano ya amani Mali

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamekariri uungaji mkono wao kwa makubaliano ya amani na maridhiano nchini Mali, huku wakielezea kutazamia utiaji saini makubaliano hayo na makundi yenye silaha mnamo Juni 20, na hivyo kukamilisha mchakato mzima wa amani na mashauriano.

Wajumbe hao wametoa wito kwa makundi hayo yenye silaha kujiepusha na  vitendo vyovyote ambavyo vinaweza kuvuruga mchakato wa amani, na kuonyesha uwajibikaji na ujasiri kwa ajili ya amani nchini Mali.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama pia wameeleza kusikitishwa na hali ya usalama ndani na karibu na mji wa Ménaka, katika mkoa wa Gao, na kutoa wito kwa makundi yaliyojihami kuondoa vikosi vyao mara moja kutoka mji wa Ménaka, na kutia saini makubaliano ya kumaliza uhasama.