Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yachukua hatua zaidi kuhibiti Kipindupindu Tanzania

WHO yachukua hatua zaidi kuhibiti Kipindupindu Tanzania

Shirika la afya duniani, WHO limehamasisha upatikanaji wa dozi 164,500 za chanjo dhidi ya Kipindupindu ili kusaidia kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo mkoani Kigoma nchini Tanzania.

Hatua hiyo inafuatia mkutano wa kamati ya afya ya mkoa huo ulioitishwa jana na mkuu wa mkoa wa Kigoma na kutangaza kampeni ya chanjo itakayotolewa kwa siku nne hasa kwenye maeneo hatarishi.

Maeneo hayo ni pamoja na vijiji vilivyo karibu na kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ambayo ujio wa wakimbizi kutoka Burundi umesababisha idadi ya wakimbizi kufikia zaidi ya 55,000.

Mwakilishi wa WHO nchini Tanzania Dkt. Rufaro Chatora chanjo hizi zitapatiwa siyo tu kwa wakimbizi walioko Nyarugusu bali pia wanavijiji wa Kagunga, Karago na Kigoma-Ujiji.

Amesema tayari watoa huduma wa ziada kutoka WHO na UNICEF wamewasili ili kusaidia maandalizi ya kampeni na hivyo iwafikie watu wengi kadri iwezekanavyo.

Tangu Kipindupindu kilipuke tarehe 10 mwezi Mei mwaka huu huko Kigoma, kutokana na wimbi la wakimbizi wa Burundi, kimesababisha vifo vya watu 34 wakiwemo watanzania watatu, kati ya wagonjwa 129 walioripotiwa.