Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili dhidi ya watoto umezidi sudan Kusini- UNICEF

Ukatili dhidi ya watoto umezidi sudan Kusini- UNICEF

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Anthony Lake amesema ukatili dhidi ya watoto umefika kiwango cha kupindukia Sudan Kusini.

Katika taarifa iliyotolewa leo, UNICEF imesema kuwa watoto wapatao 129 kutoka jimbo la Unity wameuawa kwa kipindi cha wiki tatu mwezi Mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa manusura wa uhalifu huo, wavulana wamekatwa sehemu zao za kiume na kuachwa kufa kwa kuvuja damu, na wasichana wamebakwa na watu wengi na kuuawa, huku wengine wakitupwa kwenye nyumba zilizoteketezwa.

Aidha UNICEF imekadiria kwamba watoto wapatao 13,000 wametumikishwa na vikundi vya wanajeshi vya pande zote za mzozo, Bwana Lake akisema kuwa vitendo hivyo vinaathiri watoto kimwili na kiakili.

Aidha Bwana Lake amesema ghasia ukatili huo unapaswa kusitishwa, kwa ajili ya maadili na utu wa binadamu.