Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 18.8 zahitajika kuwasaidia watu milioni 78.9- O'Brien

Dola bilioni 18.8 zahitajika kuwasaidia watu milioni 78.9- O'Brien

Mratibu Mkuu wa masuala ya Kibinadamu na misaada ya Dharura katika Umoja wa Mataifa, Bwana Stephen O’Brien amesema leo kuwa dola bilioni 18.8 zinahitajika sasa hivi ili kukidhi mahitaji ya watu milioni 78.9 katika nchi 37, lakini kufikia sasa, ni asilimia 26 tu fedha hizo ndizo zimepokelewa na mashirika ya kibinadamu.

Akihutubia kikao cha Baraza la masuala ya kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi,  Bwana O’Brien amesema zaidi ya watu milioni 110 hutegemea mashirika ya kibinadamu kwa usaidizi wa kunusuru maisha na ulinzi.

Amesema nchini Yemen, watu milioni 20, sawa na asilimia 80 ya idadi ya watu, wanahitaji usaidizi wa kibinadamu, huku watu milioni 12.2 wakihitaji usaidizi kama huo nchini Syria. Aidha, amesema nchini Sudan Kusini milioni 4.6 sasa wanakabiliwa uhaba wa chakula uliokithiri, huku watu milioni 1.3 wakiwa wamelazimika kukimbia mapigano nchini Ukraine.

Hata hivyo, amesema ingawa hatma ya watu katika nchi hizo zilizotajwa inajulikana sana, tatizo la kibinadamu kwenye ukanda wa Sahel limesahauliwa.

“Ni nadra kusikia kuhusu hatma ya watu wapatao milioni 20 wanaokabiliwa na hatari ya njaa kwenye ukanda wa Sahel, wakiwemo watoto milioni 1.4 chini ya umri wa miaka 50 walio na utapiamlo uliokithiri.

Aidha amesema, hizi zote si takwimu tu..

“Kila moja ya takwimu hizi, inawakilisha janga la kibinafsi kwa mtu fulani: kutenganishwa na makazi na jamii; kukosa elimu; kushindwa kupanda mbegu za mazao yam waka ujao; maisha ya misukosuko na sintofahamu

Ametaja baadhi ya sababu za kuongezeka mahitaji ya kibinadamu, zikiwemo ghasia za mijini, kuongezeka safari za uhamiaji, athari za mabadiliko ya tabianchi na milipuko ya magonjwa kama Ebola na Chikungunya.