Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwekeze katika udongo, tulinde haki ya kuwa na chakula- Ban

Tuwekeze katika udongo, tulinde haki ya kuwa na chakula- Ban

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya kupambana na kuenea kwa jangwa na ukame, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema uharibifu wa ardhi na kuenea kwa jangwa kunavuruga kufurahia haki za binadamu, ikiwemo haki ya kuwa na chakula. Taarifa kamili na Joshua Mmali

Taarifa ya Joshua

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii, Ban amesema takriban watu bilioni moja hawana lishe ya kutosha, na walioathirika zaidi ni wale wanaoishi kwenye ardhi iliyoharibiwa au kwenye ukame.

Katibu Mkuu amesema hali hii inaweza kuzorota zaidi iwapo uharibifu wa ardhi utapunguza uzalishaji wa chakula kwa asilimia 12 ifikapo mwaka 2035.

Akiongeza kuwa uhakika wa kuwa na chakula huathiriwa na kupungua kwa rasilmali za maji pale ardhi inapoharibiwa, Katibu Mkuu ametoa wito wa kuwekeza katika udongo ili kulinda haki ya kuwa na chakula na maji safi.

Louise Baker ni afisa wa sera kwenye Sekritariati ya Mktaba wa kupambana na kuenea kwa jangwa. Katika mahojiano na idhaa hii, ameeleza ukubwa na athari za kuenea kwa jangwa...

“Duniani, kuna takriban ekari bilioni mbili za ardhi iliyoharibiwa, na kati ya hiyo, karibu ekari milioni 500 haitumiki tena kabisa. Hasara yake kiuchumi ni dola bilioni 40 kila mwaka, lakini pia kijamii, hasara yake ni kubwa, katika kuzalisha chakula, upatikanaji wa maji, na kulazimu watu kuhama pale mazao ya ardhi yao yanapopungua.”