Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baba anayelea mwanae anaepuka madhila mengi ikiwemo magonjwa

Baba anayelea mwanae anaepuka madhila mengi ikiwemo magonjwa

Ripoti ya kwanza kabisa kuhusu hali ya akina baba duniani imezinduliwa jijini New York, Marekani ikisema hadi sasa hakuna nchi ambayo kwayo jukumu la malezi ya watoto ambalo halina ujira wowote linajumuisha sawia baba na mama na hivyo kusababisha baba kutokuwepo kwenye malezi ya mtoto wake. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Akizungumza kwenye uzinduzi huo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA Kate Gilmore amesema jambo hilo lina madhara kwa kuwa ripoti imebaini kuwa..

(Sauti ya Kate)

“Wanaume wenye uhusiano mzuri wa karibu na watoto wao ambao hauna ghasia wanaishi muda mrefu zaidi na wana maradhi madogo sana ya kimwili na kiakili. Pia wana fursa ndogo sana ya kuwa tegemezi wa madawa ya kulevya na pia wanakuwa na ufanisi zaidi kazini. Wavulana na wasichana wanaokosa malezi ya baba wanapata hasara pia.”

Ripoti hiyo imetajwa kuwa ni muhimu zaidi wakati huu ambapo asilimia 80 ya wanaume na wavulana watakuwa na jukumu la baba katika maisha yao na hivyo ni vyema kuweka mazingira ambayo kwayo wataweza kushiriki vyema katika kujenga uhusiano bora na watoto wao.