Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo huru lapendekeza kubadilisha mfumo wa ulinzi wa amani wa UM

Jopo huru lapendekeza kubadilisha mfumo wa ulinzi wa amani wa UM

Jose Ramos Horta, mwenyekiti wa jopo huru lililowasilisha leo ripoti yake kuhusu operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa ametangaza mapendekezo muhimu ya ripoti hiyo iliyoandaliwa na watu 15 baada ya miezi nane ya utafiti na safari mbali mbali ikiwemo nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini New York, Marekani, Bwana Horta ametaja mapendekezo manne ya msingi kuwa ni pamoja na kuweka kipaumbele katika suluhu za kisiasa badala ya suluhu za kijeshi, akisema:

“ Amani haiwezi kufikiwa wala kudumu kupitia mapigano ya kijeshi pekee, lakini mara nyingi suluhu hupatikana kupitia mazungumzo ya kisiasa. Kwa hiyo lazima operesheni za amani ziongozwe na kipaumbele cha siasa” .

Pendekezo lingine ni kuimarisha uwezo wa operesheni za ulinzi wa amani wa kubadilika kwa haraka kulingana na mazingira.

Halikadhalika, Bwana Horta ambaye pia ni Rais wa zamani wa Timor Letes, amesema wamezingatia umuhimu wa ushirikiano na mashirika ya kikanda, hasa Muungano wa Afrika, na pendekezo la mwisho ni kulenga zaidi mahitaji yaliyopo kwenye maeneo ya operesheni zenyewe na mahitaji ya raia.

Miongoni mwa mapendekezo muhimu mengine yaliyotolewa ni kuunda mfumo mdogo wa dharura kwa ajili ya kuweza kutuma walinda amani kwa haraka iwapo mzozo unapoibuka na kwamba jopo limeshauri walinda amani wajizuie kupigana hasa mapigano ya moja kwa moja na vikundi vya kigaidi kwa kuwa hayo si majukumu ya Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo Bwana Horta ametaka ripoti isipatiwe jina lake, bali ipatiwe jina la mtoto mdogo wa kike kutoka Sudan Kusini aliyetembea kilomita nyingi kutafuta msaada kwa ajili ya baba yake mzazi, akisema mtoto huyo ni mfano mzuri kwake wa kupambana na athari za vita na kubaki na matumaini.