Ban asikitishwa na hukumu ya kifo kwa Morsi na wengine Misri

16 Juni 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameeleza kusikitishwa sana na hukumu ya kifo iliyotolewa kwa washukiwa wapatao 100 nchini Misri, akiwemo rais wa zamani, Mohamed Morsi.

Taarifa ya msemaji wake imesema Umoja wa Mataifa unapinga matumizi ya hukumu ya kifo katika mazingira yoyote yale. Taarifa hiyo imemnukuu Ban akitoa wito kwa serikali ya Misri kuridhia mkataba wa pili wa kimataifa kuhusu haki za umma na kisiasa, na kusitisha utekelezaji wa hukumu ya kifo.

Ban ameeleza hofu yake kuwa hukumu kama hiyo inayotolewa baada ya kesi ya halaiki, inaweza kuathiri vibaya matumaini ya ustawi wa muda mrefu nchini Misri. Amesisitiza umuhimu wa kuruhusu sauti zote kusikika na kuwakilishwa, na kutoa wito kwa mamlaka za Misri kuhakikisha kuwa washukukiwa wananufaika na mchakato unaoweza kuhakikisha haki na kutodhulumiwa kisheria.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter