Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia Sudan Kusini yaongeza mahitaji ya kibinadamu: OCHA

Ghasia Sudan Kusini yaongeza mahitaji ya kibinadamu: OCHA

Leo mjini Geneva, Uswisi kumefanyika mkutano maalum kuhusu mzozo wa kibinadamu nchini Sudan Kusini ambapo Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, Stephen O’Brien amesema mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka huku mapigano yakiendelea na hata kuongezeka nchini humo.

Ameeleza kwamba idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu imeongezeka maradufu tangu mwanzo wa mwaka huu na kufika milioni 4.6 na kwamba wakati huu ambapo msimu wa mvua unakaribia, hatari za magonjwa kama malaria au kipindupindu zinaongezeka, huku huduma za afya, maji safi na kujisafi zikikaribia kufilisika.

Halikadhalika amemulika wahudumu wa kibinadamu ambao wanafanya kazi kwenye mazingira magumu, ambapo miongoni mwao 13 wameuawa tangu mwanzo wa mzozo huu.

Hata hivyo amesema, msaada wa kibinadamu umekuwa na ufanisi nchini humo, watu milioni 3.6 wakiwa wamesaidiwa mwaka 2014.

Hatimaye akatoa mapendekezo matatu: jamii ya kimataifa ishawishi pande za mzozo kusitisha mapigano, pande za mzozo ziheshimu haki ya kimataifa ya kibinadamu ili kulinda wahudumu wa kibinadamu, na mwishowe, miradi ya usaidizi wa kibinadamu ipatiwe ufadhili unaotakiwa.

Wakati huo huo, Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, amefafanua mahitaji ya fedha kwa Sudan Kusini:

Ombi la fedha lililoangaliwa upya linasaka dola bilioni 1.63 ili kutimiza mahitaji ya dharura zaidi mpaka mwisho wa mwaka, na pengo ni la dola bilioni moja kwa sasa.”