Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia Yemen yahatarisha mustakhabali wa watoto: UNICEF

Ghasia Yemen yahatarisha mustakhabali wa watoto: UNICEF

Nchini Yemen, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limeelezea wasiwasi wake kuhusu idadi kubwa ya watoto wanaouawa, kujeruhiwa au kutumikishwa jeshini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, Uswisi msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac amesema tangu mwanzo wa mzozo nchini Yemen, tarehe 26 Machi mwaka huu, watoto 279 wameuawa, 402 kujeruhiwa na 318 kutumikishwa jeshini.

Bwana Boulierac amesema idadi hii ni zaidi ya mara nne ile ya mwaka 2014.

“ Watoto wanaendelea kuuawa, kulemazwa, au kutumikishwa vitani. Wangepaswa kusoma shuleni kwa usalama, sio kukimbia risasi vitani. Watoto hao ni mustakhabali wa Yemen na wanapaswa kulindwa muda wote na maumivu »

Amesema UNICEF imekaribisha wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano wakati wa mwezi wa Ramadhan ili kufikisha misaada ya kibinadamu.