Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apokea ripoti ya tathmini ya operesheni za ulinzi wa amani za UM

Ban apokea ripoti ya tathmini ya operesheni za ulinzi wa amani za UM

Jopo huru la ngazi ya juu lililoundwa kutathmini operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa limehitimisha jukumu hilo na kukabidhi rasmi ripoti kwa katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon jijini New York, Marekani.

Mwenyekiti wa jopo hilo Jose Ramos-Horta na makamu wake Bi. Ameerah Haq, wamekabidhi ripoti hiyo baada ya tathmini ambayo imeelezwa na Ban kuwa ni ya kina ikijumuisha pande mbali mbali wakati huu ambapo operesheni za ulinzi wa amani zinafanyika kusiko na amani.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa, Ban amesema ataisoma kwa kina na kuwasilisha kwa wadau wote mapendekezo hayo hatimaye ili operesheni za ulinzi wa amani ziwe na tija siyo tu kwa Umoja wa Mataifa bali pia kule zinakofanyika.

Jopo hilo liliundwa mwezi Oktoba mwaka jana na miongoni mwa majukumu ni kutathmini operesheni za sasa za amani za Umoja wa Mataifa na mahitaji yanayoweza kuibuka siku za usoni.

Baadaye leo, Bwana Horta ambaye ni Rais wa zamani wa Timor Letse, ataweka bayana mapendekezo hayo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jijini New York.