Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ya wasichana ni ufunguo wa maendeleo ya jamii: Zeid

Elimu ya wasichana ni ufunguo wa maendeleo ya jamii: Zeid

Leo kwenye mjadala maalum kuhusu kutimiza haki sawa ya kupata elimu kwa wasichana wote uliofanyika mjini Geneva, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad al Hussein amesema elimu ya wasichana ni ufunguo wa maendeleo ya jamii nzima. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Kamishna Zeid amekaribisha mafanikio yaliyopatikana katika kutimiza lengo namba tatu la maendeleo ya milenia kuhusu usawa wa kijinsia katika elimu, akisema katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita wanawake na wasichana wengi wamepatiwa fursa na hivyo kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kujitegema, kuongoza maisha yao na kushiriki kwenye jamii.

Hata hivyo, amesikitishwa na changamoto ambazo bado zinakumba elimu ya wasichana zikiwemo mashambulizi ya kigaidi, ubaguzi, ukatili wa kingono au ukosefu wa usawa katika kupewa fursa za ajira.

Amesisitiza kwamba elimu ya wasichana ni ufunguo unaoweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii, ikiwa ni kwa upande wa ukuaji wa uchumi, usalama wa nchi au afya ya watoto, akisema

“ Kuwekeza katika elimu ya wasichana sio tu ni jambo sahihi, bali pia ni jambo la maana zaidi. Hakuna jamii inayoweza kutimiza mafanikio iwapo itazuia nusu ya raia yake kujiendeleza. Elimu ya wasichana ni hatua ya kwanza, inaweza kubadilisha mitazamo, kuendeleza jamii na kuimarisha mamilioni ya maisha.”