Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mrithi wa Kutesa Baraza Kuu ateuliwa, ni Mogens Lykketoft kutoka Denmark

Mrithi wa Kutesa Baraza Kuu ateuliwa, ni Mogens Lykketoft kutoka Denmark

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa leo jumatatu limeridhia uteuzi Mogens Lykketoft  kutoka Denmark kuwa Rais wa mkutano wa 70 wa baraza hilo.

Akiongea baada ya uteuzi huo rasmi Rais huyo mpya wa Baraza Kuu atakayeanza kutekeleza majukumu yake mwezi Septemba mwaka huu amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kukabiliwa na changamoto ya kusongesha juhudi za amani na maendeleo endelevu hivyo akashauri kuwa..

(SAUTI MOGENS)

‘‘Ili kufanikiwa lazima tujitahidi kujenga dunia ya haki na thabiti zaidi, na kila mmoja wetu lazima atimize wajibu wake. Nchi wahisani lazima zitoe ahadi zake kwa ajili ya maendeleo. Nchi zote lazima ziimarishe matumizi ya rasilimali ili kufikia mahitaji’ ya kimaendeleo’.

Kiongozi huyo ambaye  anatarajia kutimiza umri wa miaka 70 baadaye mwaka huu sanjari na Umoja wa Mataifa na hivyo kuongoza mkutano huo wa 70 amesema anatarajia kuongoza kikao cha baraza chini ya kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa miaka 70 ahadi mpya ya utekelezaji ikijielekeza katika mafanikio, changamoto na mipango ya baadaye.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ban ki-Moon akimkaribisha  Bwana Lykketoft ambaye ni spika wa zamani wa Bunge la Denmark, amesema ataongoza baraza kuu katika mwaka muhimu ikiwa ni hitimisho la mipango ya maendeleo ya milenia na hivyo

(SAUTI BAN)

‘‘Pamoja tunaweza kufanya kazi ili Umoja wa Mataifa utimize matakwa yake kwa mwaka huu na kuhakikisha mustakabali mwema wa dunia yetu’’.

Bwana Ban awali amemepongeza Rais huyo mpya wa baraza kuu na kuelezea imani ya UM kuhusu uongozi wake.