Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola Bilioni 109 zatumwa na wahamiaji wa Ulaya mwaka jana pekee

Dola Bilioni 109 zatumwa na wahamiaji wa Ulaya mwaka jana pekee

Wahamiaji walioko barani Ulaya, mwaka jana pekee walituma zaidi ya dola Bilioni 109 kwenda kwa familia zao maeneo mbali mbali duniani.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo kuhusu utumaji fedha nyumbani iliyotolewa na shirika la kimataifa la maendeleo ya kilimo, IFAD.

Rais wa IFAD Kanayo Nwanze amesema ingawa kiwango hicho ni robo tu ya fedha zinazotumwa duniani kote, muhimu ni kwamba zinanufaisha familia za wahamiaji nyumbani na kingaliweza kuwa cha juu zaidi iwapo kungalikuwepo na mbinu rahisi na nafuu zaidi za kuwawezesha kuweka akiba na kuwekeza.

Bwana Nwanze amesema ni vyema kuhakikisha fedha hizo zinazopatikana kwa kufanya kazi kwa bidii zinatumwa nyumbani kwa unafuu lakini zaidi zinawezesha jamii kujikwamua hususan kwenye jamii maskini zaidi ambako ndiko fedha zinatumwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo nchi zinazoongoza kwa kutuma fedha nyingi ni Urusi, Uingereza, Ujerumani, Italia na Hispania.