Skip to main content

Yemen yateketea, asema Ban Ki-moon

Yemen yateketea, asema Ban Ki-moon

Wakati mashauriano ya amani kuhusu Yemen yameanza leo mjini Geneva, Uswisi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema Yemen inahitaji usaidizi hara iwezekanavyo.

Amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mjini humo, akiongeza kwamba ni wajibu wa pande zote kwenye mzozo kusitisha mapigano na ni wajibu wa jamii ya kimataifa kusaidia jitihada hizo.

Tunapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya raia wa Yemen, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya raia sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu. Hatuna muda wa kupoteza. Mapigano yanakipatia nguvu zaidi baadhi ya vikundi vya kigaidi katili zaidi duniani”.

Huku akisema kwamba ukanda wa Mashariki ya Kati hauwezi kuvumilia mzozo mwingine kama ule wa Libya au Syria, ameziomba pande za mzozo zikubali kusitisha mapigano kwa ajili ya mahitaji ya kibinadamu wakati huu ambapo mwezi wa Ramadhan unaanza, pia kusitisha mapigano kwenye baadhi ya maeneo, na hatimaye kuanza tena utaratibu wa mpito wa kisiasa.