Skip to main content

De Mistura akaribisha mwaliko wa serikali ya Syria kuzuru Damascus

De Mistura akaribisha mwaliko wa serikali ya Syria kuzuru Damascus

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, amekubali mwaliko wa serikali ya Syria wa kuzuru Damascus.

Katika taarifa, Bwana de Mistura amesema anatazamia kukutana na maafisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Syria, akilenga kuwapa fursa ya kutoa maoni yao kuhusu mashauriano ya Geneva, ambayo yalianza mapema mwezi Mei na yataendelea hadi Julai.

Katika ziara hiyo, de Mistura anatarajia kuzungumza na serikali kuhusu suala la kuwalinda raia, na kusisitiza kuwa haikubaliki kutumia mabomu katika maeneo ya raia, na kwamba serikali ina wajibu wa kuwalinda raia katika mazingira yoyote yale, chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Bwana de Mistura pia amepanga kujadili kuhusu hali ya kibinadamu ya hivi sasa Syria, na jinsi ya kuongeza uwezo wa kuzifikia jamii zilizozingirwa, na kusisitiza kuwa suluhu kwa mzozo wa Syria haliwezi kupatikana kwa lazima, na kwamba suluhu jumuishi la kisiasa, linaloongozwa na WaSyria wenyewe linahitajika haraka sana.