Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-Moon ataka kupambana na ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi

Ban Ki-Moon ataka kupambana na ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya uelewa kuhusu albinism, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema sasa ni wakati wa kuondoa imani potofu na kuhakikishia haki za watu wenye ulemavu wa ngozi, albinism.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo, Bwana Ban amesema watu wenye ulemavu wa ngozi wanaweza kuishi maisha ya kawaida wakipewa fursa sawa, lakini mara nyingi bado wanatengwa, kubaguliwa, hadi kujeruhiwa na kuuawa.

Bwana Ban ameeleza kutiwa wasiwasi na ripoti za mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, wakiwemo watoto, wanawake na watu wenye ulemavu.

Amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kuhamasisha jamii ili kupambana na ubaguzi, huku akizisihi nchi wanachama kuchukua hatua zote kulinda watu wenye ulemavu, kuwapa huduma zote wanazohitaji, kupambana na ubaguzi na kupeleka wetekelezaji wa uhalifu dhidi ya watu hao mbele ya sheria.