Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashauriano kuhusu Yemen kuanza Geneva Jumapili, Ban kuhudhuria

Mashauriano kuhusu Yemen kuanza Geneva Jumapili, Ban kuhudhuria

Mashauriano kati ya pande kinzani nchini Yemen yanatarajiwa kuanza Jumapili hii huko Geneva, Uswisi ikiwa ni n’gwe nyingine ya kujaribu kumaliza mzozo unaoendelea nchini humo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anatarajiwa kufungua mashauriano hayo yatakayoongozwa na mjumbe wake maalum huko Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed.

Mkurugenzi wa habari kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Ahmad Fawzi amesema mashauriano hayo ni sehemu ya mchakato wa amani na kwamba ni hatua muhimu sana kwani ni ya kwanza kuhusisha pande mbali mbali tangu chuki zilivyoanza tena nchini Yemen.

Amesema kwa mantiki hiyo yatakuwa ni sehemu muhimu na ni matumaini  yao kuwa pande hizo zitashiriki vyema ili kuanza mwelekeo wa kumaliza tofauti zao.

Washiriki ni pamoja na wajumbe wa baraza la ushirikiano wa ghuba, GCC, na kutoka Riyadh na Sana’a. Halikadhalika kundi la nchi 16, G16 ambazo ni pamoja na China, Ufaransa, Urusi na Marekani.