Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwait yatoa dola milioni $120 kusaidia operesheni za kibinadamu Syria

Kuwait yatoa dola milioni $120 kusaidia operesheni za kibinadamu Syria

Kuwait imetoa dola milioni 121 kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, ili kusaidia juhudi za shirika hilo za kukabiliana na tatizo la kibinadamu nchini Syria.

Akiipokea hundi ya mchango huo kutoka kwa Bwana Abdullah Al Matouq, ambaye ni mshauri wa Mtawala wa Kuwait, Sheikh Sabah Al-Ahmed Al-Jaber Al-Sabah, Kamishna Mkuu wa UNHCR, António Guterres amemshukuru na kumsifu Mtawala huyo wa Kuwait, serikali na watu wake kwa ukarimu wao mkubwa.

Guterres amesema, wakati huu mwezi wa Ramadan unapokaribia, hakuna kitu kilicho bora kuliko hafla ya utoaji mchango huo, ambayo ni ya kusherehekea ukarimu ambao ni sehemu ya Uislamu.

Fedha hizo, ambazo ni sehemu ya ahadi ya mchango wa dola milioni 500 iliyotoa Kuwait katika kongamano la mwezi Machi katika mji wa Kuwait, utatumiwa katika nchi jirani za Syria kuwapa ahueni WaSyria milioni 3.9 wanaoteseka, katika sekta mbalimbali.