Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani kuharibiwa kwa mji wa kihistoria wa Sana’a nchini Yemen

UNESCO yalaani kuharibiwa kwa mji wa kihistoria wa Sana’a nchini Yemen

Shirikila la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO limelaani kuharibiwa kwa mji wa kihistoria wa Sana’a nchini Yemen ambao uko katika orodha ya urithi wa dunia.

Mkurugenzi mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema nyumba kadhaa zimeharibiwa na kusababaisha majeruhi mjini humo baada ya bomu kulipuka mnamo June 12 mwaka huu, miongoni mwa majengo yaliyoliharibika ni jumba la asili lililoko Al Qasimi na ambalo linapakana na bustani iliyoko mjini iitwayo Miqshama karibu na mfereji wa maji wa Sailah.

Amesema mji huo umedumu na wenyeji wake kwa zaidi ya  miaka 2,500 na kushuhudia utajiri na uzuri wa ustaarabu wa kiisalamu na kwamba katika karne ya kwanza Sana’a ilikuwa kituo cha njia ya biashara ya bara huku nyumba na majengo ya kijamii yakisalia mifano halisi ya utamaduni na makazi ya kiisalamu.

UNESCO imesema tangu kuanza kwa machafuko nchini Yemen uharibifu kadhaa umeshuhudiwa na hivyo kuondoa thamani ya historia na kumbukumbu katika eneo huku ikisema uharibifu huo haukarabatiki.