Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na EU zawekeza katika huduma za msingi kwa watoto CAR

UNICEF na EU zawekeza katika huduma za msingi kwa watoto CAR

Miradi miwili mikubwa imezinduliwa leo na Muungano wa Ulaya, Wizara za Elimu na Afya za Jamhrui ya Afrika ya Kati pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudhumia Watoto UNICEF, ikilenga kurejesha huduma za elimu na afya kwa watoto kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na mzozo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na UNICEF, mradi wa elimu wa euro milioni 21 unalenga kukarabati shule 300, kutoa mafunzo kwa walimu au kurejesha shuleni watoto waliotumukishwa jeshini.

Mradi wa afya wenye thamani ya euro milioni 4.5 unaofadhiliwa na UNICEf na Muungano wa Ulaya utalenga watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ili kutibu utapiamlo, malaria na ugonjwa wa kuhara.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, msemaji wa UNICEF. Christophe Boulierac amesema mzozo umeathiri sana huduma za afya na elimu nchini CAR, mtoto mmoja kati ya watatu akiwa haendi shuleni.

"Watoto wameteseka sana na mzozo huu na mpaka sasa hivi wanateseka. Kwa hiyo tunapaswa kujenga nchi upya, tunaanza kwa chini saana. Jamhuri ya Afrika ya Kati inaelekea kwenye njia ya amani, kwa hiyo sasa tunapaswa kujenga upya huduma za msingi za kijamii.”