Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msimu wa mwambo wasababisha wakimbizi kurejea kambini:WFP

Msimu wa mwambo wasababisha wakimbizi kurejea kambini:WFP

Msimu wa mwambo ukikaribia huko Cameroon, maelfu ya wakimbizi kutoka Nigeria,  ambao walikuwa wamepatiwa hifadhi na wenyeji, wameamua kuelekea kwenye kambi ya wakimbizi ya Minawao tangu mwishoni mwa mwezi uliopita.Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Wakimbizi hao na wale wa ndani waliokuwa wamerejea nyumbani wanasema wameamua kuondoka kwa kuwa hawana uhakika wa chakula kwani hata wenyeji wanashindwa kukidhi mahitaji yao kutokana na ukosefu wa chakula.

Kutokana na hali hiyo shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linatiwa hofu wakati huu ambapo mashambulizi ya Boko Haram yanatishia kuongeza idadi zaidi ya wakimbizi kwa hiyo Elizabeth Byrs msemaji wa shirika hilo anasema wanachofanya..

“Msimu wa mvua ukikaribia, vituo vya afya tayari vinahaha kukidhi mahitaji. WFP inalenga kusaidia watu Laki Nne kila mwezi lakini hatuwezi bila fedha. WFP imechangiwa chin ya asilimia 50 tukihitaji dola Milioni 41 nukta Sita hadi mwisho wa mwaka huu.”

Ghasia za Boko Haram zimesababisha mipaka kufungwa na hivyo kukwamisha biashara, wafugaji kushindwa kulisha mifugo yao na hata kupigwa marufuku kwa shughuli za uvuvi huko Chad kwa sababu za usalama.