Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pakistan sitisha hukumu ya kifo: Kamishna Zeid

Pakistan sitisha hukumu ya kifo: Kamishna Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ametoa wito kwa serikali ya Pakistani kurejesha tena amri ya kuzuia hukumu ya kifo.

Awali nchi hiyo ilikuwa imesitisha adhabu hiyo lakini ilirejeshwa kufuatia shambulio dhidi ya shule huko Peshawar mwezi Disemba mwaka jana.

Katika ombi lake alililotoa leo, Kamishna Zeid amesema tangu kuondolewa kwa sitisho hilo, zaidi ya watu 150 wakiwemo watoto wameuawa, kitendo ambacho amesema kinasikitisha licha ya kwamba hata mauaji  ya watu 145 wakiwemo wanafunzi huko Peshawar nayo yalitia machungu na anatambua hali hiyo.

Amesema kutekelezwa kwa adhabu ya kifo kwa watu 154 ndani ya kipindi cha miezi Sita ni idadi kubwa sana hivyo kufanya nchi Tatu duniani kwa kutekeleza kuua watu wengi kupitia adhabu ya kifo.

Kamishna Zeid amekumbusha kuwa mauaji ya watu wengi kupitia adhabu  hiyo siyo suluhu la kumaliza uhalifu kama vile mauaji ya Peshawar lakini yanaweza kutumiwa na watu wenye misimamo mikali kuelezea kuwa ni ukiukaji wa haki na hivyo kuhadaa vijana  wajiunge nao.

Kwa sasa nchini Pakistani watu 8,000 wanasubiria kuuawa ambapo kati ya 800 ni wafungwa ambao yadaiwa walitenda makosa yao wakiwa watoto.