Skip to main content

Msuluhishi wa mzozo Burundi ajiondoa.

Msuluhishi wa mzozo Burundi ajiondoa.

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi za maziwa makuu, Said Djinnit amejiotoa katika ushiriki wake wa kuongoza mashauriano ya amani nchini Burundi, mchakato alioongoza tangu mwezi Aprili mwaka huu baada ya ghasia kuibuka nchini humo.

Hatua hiyo inakuja kufuatia upinzani kutoka kwa pande mbali mbali nchini humo ikiwemo mashirika ya kiraia, kwa mujibu wa msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, MENUB, Vladmir Monteiro.

(Sauti ya Vladmir)

"Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kupitia taarifa iliyotolewa Jumatano alikubali ombi lililotolwa na vyama mbalimbali vya upinzani na vyama vya kiraia katika jukumu la kuratibu mazungumzo ya amani, ningependa kukumbusha kwamba amekuweop Burundi tangu Aprili kufuatia uteuzi wake kufuatilia hali nchini Burundi. Alipata vitisho vingi lakini licha ya kuondoka kwake bado anajali Burundi kwa mamlaka yake kama Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kwa Maziwa Makuu."

Akizungumza na waandishi wa habari mchana huu, msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amethibitisha hatua ya Djinnit kujitoa katika mazungumzo hayo na kusalia mjumbe maaluk kwa Maziwa Makuu, akiweka matarajio  ya Umoja huo kwa mkutano wa viongozi wa Muungano wa Afrika tarehe 14 na 15 mwezi huu huko Afrika Kusini.

(Sauti ya Dujarric)

"Tutashauriana na viongozi wa ukanda wa maziwa makuu, Kamisheni ya Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na mkutano wa kimataifa kuhusu maziwa makuu kuona ni jinsi gani Umoja wa Mataifa unaweza kuendelea kusaidia jitihada za kimataifa za kushawishi mashauriano ya kisiasa baina ya wadau wote nchini Burundi. Umoja wa Mataifa unaamini kuwa hilo litakuwa ni ajenda kwenye mjadala wa mkutano wa viongozi wa Muungano wa Afrika. Tutakuwa na taarifa zaidi kuhusu hali ilivyo ikiwemo jukumu la mwezeshaji baada ya mashauriano hayo.”

Burundi ilitumbukia katika sintofahamu baada ya Rais Pierre Nkurunzinza kutangazwa kuwania nafasi ya urais kwa awamu ya tatu mwezi Aprili mwaka huu na kusababisha watu wapatao Laki Moja kukimbilia nchi jirani kusaka hifadhi.