Mwakilishi wa UM Iraq alaani kampeni ya ISIL ya kuwatisha raia

10 Juni 2015

Leo ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kundi la kigaidi la ISIL kutwaa mji wa Mosul nchini Iraq, kundi hilo limeendelea kuharibu maisha ya mamilioni ya raia, hasa vikundi vya walio wachache, kutekeleza uhalifu ambao unaweza kubainiwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu wa kibindamu, pamoja na kuharibu urithi wa dunia.

Hii ni kwa mujibu wa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Jan Kubis, akisema vitendo hivyo vinaonyesha haja ya kupambana na kundi hilo, lakini pia kuendelea na mazungumzo jumuishi ya kisiasa nchini humo, kwa ajili ya maridhiano.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Bwana Kubis amesema kundi la ISIL ni tishio kubwa kwa usalama na amani ya kimataifa, na linahitaji hatua ya pamoja ili kupambana nalo.

Aidha amemulika hali ya kibinadamu, akisema mtu mmoja kati ya wanne Iraq anahitaji msaada wa kibinadamu, wakiwemo wakimbizi wa ndani milioni 3.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter