Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano kati ya MONUSCO na jeshi la DRC umefana: Kobler

Ushirikiano kati ya MONUSCO na jeshi la DRC umefana: Kobler

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, Martin Kobler ametangaza leo kwamba operesheni ya pamoja ya MONSUCO na jeshi la kitaifa la DRC imefanikiwa kupambana na waasi wa FRPI waliopo kwenye maeneo ya Ituri mashariki mwa nchi.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Kobler amesema mafanikio hayo ni dalili inayoonyesha faida ya ushirikiano kati ya MONUSCO na FARDC.

"Tukiungana kwa ukweli na FARDC, tukiweza kusaidia FARDC, inafaa, na inaleta mafanikio. Tuko na ndege zisizo za rubani na helikopta za kushambulia. Kwa kweli tumepigana pamoja tukiwa na mpango wa pamoja, tumepigana dhidi ya FRPI chini ya uongozi wa FARDC na kwa ufanisi kwa kusema kweli"

Operesheni hiyo ya pamoja imeanzishwa wiki moja iliyopita baada ya waasi wa FRPI kukataa kujisalimisha, huku mkuu wa MONUSCO akieleza kwamba kwa kipindi cha siku moja tu tarehe 8 mwezi Juni, waasi 34 wameuawa, 24 kujeruhiwa na wengine 8 kukamatwa na FARDC.

Aidha Bwana Kobler amepongeza kikosi cha walinda amani wa Bangladesh ambao wamejitahidi katika operesheni hizi za kijeshi pamoja na kuhakikisha usalama wa raia, huku MONUSCO ikisema kuwa baadhi ya wakazi waliopo kwenye maeneo ya mapigano walilazimika kukimbia.

Hatimaye bwana Kobler amekariri wito wake kwa waasi wa FRPI akisema bado wanaweza kujiunga na mfumo wa kujisalimisha na kuunganishwa tena na jamii, DDR.