Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu jumuishi kwa mzozo wa Syria ni muhimu: de Mistura

Suluhu jumuishi kwa mzozo wa Syria ni muhimu: de Mistura

Ikiwa ni wiki ya tano sasa tangu kuanza kwa mashauriano yenye lengo la kupatia suluhu la kudumu mzozo wa Syria, mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mistura amesema mchakato wa siasa jumuishi ndio mwarobaini wa mazungumzo hayo.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi kunakofanyika mashauriano hayo,  de Mistura ambaye ameshakuwa na vikao na wawakilishi wa serikali ya Syria, upinzani na vikundi vya kiraia na kisiasa kutoka Syria tangu tarehe Tano mwezi huu, amesema bado ana matumaini kuwa iko siku mapigano yatakoma nchini humo.

Amesema hatua hiyo haikwepekwi kwa kuwa imeshuhudiwa pia kwenye maeneo mengine ya mizozo.

Hata hivyo amesema ni wajibu wa wadau wote wa kitaifa, kikanda na kimataifa kufanikisha matamanio hayo na kuhakikisha usalama wa raia ni kipaumbele wakati wowote.

Bwana de Mistura amesema kuna makubaliano ya pamoja kuwa hakuna suluhu la kijeshi kwenye mzozo wa Syria lakini ni mchakato unaongozwa na wasyria wenyewe ndio unaoweza kumaliza mzozo huo kwa njia endelevu.