Chonde chonde serikali ya Sudan ipatie amani fursa Darfur: UNAMID
Wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikutana leo kwa mashauriano ya faragha kuhusu operesheni za ujumbe wake wa pamoja na Muungano wa Afrika huko Darfur, UNAMID, imeelezwa ukosefu wa ushirikiano kutoka serikalini kunazidi kuzorotesha operesheni hizo. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.
(Taarifa ya Grace)
Kikao hicho cha faragha kitahutubiwa na Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye operesheni za ulinzi wa amani Edmund Mulet wakati huu ambapo ripoti ya Katibu Mkuu kwa mujibu wa UNAMID inasema mchakato wa amani umekwama, huku harakati za kulinda raia ukiendelea licha ya changamoto.
Akizungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa kuhusu ripoti hiyo, Kaimu Mkuu wa UNAMID Abiodun Bashua ametaja changamoto kuwa ni kushindwa kufikia wanaohitaji misaada ya kibinadamu hasa kwenye mapigano, na nyingine ni mizozo ya kikabila ambayo UNAMID haina uwezo wa kumaliza bali inaweza kusaidia harakati za kudhibiti lakini….
(Sauti ya Bashua)
“Kwa bahati mbaya kuna watu serikalini ambao wanadhani kwamba tunashiriki na kujaribu kusaidia kupunguza mizozo ya kikabila kwa kuwa tunataka kuongeza muda wa mamlaka ya UNAMID, jambo ambalo halina maana yoyote.”
Amesema kitendo cha serikali kutoamini UNAMID tangu mwanzoni, kinasababisha kila harakati kukumbwa na shuku na hivyo kukwamisha harakati za ulinzi wa raia.