Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutesa ahitimisha ziara yake Algeria, akutana na Rais Bouteflika

Kutesa ahitimisha ziara yake Algeria, akutana na Rais Bouteflika

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa amehitimisha ziara yake rasmi nchini Algeria kwa kuwa na mazungumzo na Rais Abdelaziz Bouteflika mjini Algiers.

Mazungumzo yao yamejikita masuala kadhaa ikiwemo yaliyojiri kwenye kikao cha 69 cha Baraza Kuu, ajenda ya maendeleo endeleve baada ya mwaka 2015, na mikutano muhimu ijayo ikiwemo ule wa mabadiliko ya tabianchi na ufadhili kwa maendeleo.

Halikadhalika wameangazia umuhimu wa kuchagiza utendaji wa Baraza kuu sanjari na marekebisho ya mfumo wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa bila kusahau masuala ya uzuiaji mizozo, amani na maendeleo hususan barani Afrika.

Kutesa amemshukuru Rais Bouteflika kwa uongozi wake hasa jukumu lake kwenye mchakato wa amani nchini Mali ambapo amewezesha kupatikana kwa mkataba wa amani unaotarajiwa kutiwa saini tarehe 20 mwezi huu.