Naibu Katibu Mkuu azingatia haki za watu wenye ulemavu

9 Juni 2015

Kila mtu ana haki sawa na jamii ya kimataifa inapaswa kutekeleza azimio hilo, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson akifungua rasmi mkutano wa Nane kuhusu haki za watu wenye ulemavu ulioanza leo jijini New York.

Bwana Eliasson amesema kusainiwa kwa mkataba wa Kimataifa wa Haki za watu wenye ulemavu mwaka 2006 umewezesha kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu swala la ulemavu, likiwa tena si swala la huduma na matibabu, lakini swala la haki.

Aidha ameongeza kuwa swala hilo ni la msingi wakati huu ambapo jamii ya kimataifa inatarajiwa kuunda ajenda mpya ya maendeleo endelevu mwezi Septemba mwaka huu, kwa kulenga maendeleo jumuishi yenye usawa wa jamii.

« Cha kusikitisha sana ni kwamba watu wenye ulemavu ni miongoni mwa watu wanaotegwa zaidi karibu duniani kote. Tunahitaji kuchukua hatua mara moja ili kupunguza utengano, ukosefu wa usawa na unyanyapaa. »

Hatimaye ameangazia unyanyapaa zaidi unaokumba wanawake na wasichana wenye ulemavu, akizingatia umuhimu wa kuimarisha mfumo wa elimu kwa watu wenye ulemavu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter