Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Côte d’Ivoire

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Côte d’Ivoire

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo wamekutana kufanya mashauriano ya wazi kuhusu hali nchini Côte d’Ivoire, ambako pia wamesikiliza ripoti ya Katibu Mkuu ya tarehe 7 Mei, 2015 kuhusu hali nchini humo, na pia taarifa zaidi kuhusu matukio makuu nchini, yakiwemo maandalizi ya uchaguzi wa urais mwezi Oktoba.

Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu imewasilishwa na Bi Aïchatou Mindaoudou, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Côte d’Ivoire, UNOCI. Bi Mindaoudou amesema ofisi yake imejitahidi kuishawishi serikali na vyama vya upinzani kuelekea kwenye barabara ya mazungumzo, na pia kuwatia moyo wananchi kuhusu juhudi za serikali za kuimarisha amani na utulivu nchini, hasa wakati huu uchaguzi unapokaribia.

“Kwa Côte d’Ivoire, uchaguzi wa Oktoba wa urais unawakilisha hatua muhimu katika kuimarisha ufanisi uliopatikana katika miaka michache iliyopita. Kama mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Côte d’Ivoire, nimehakikisha kuimarishwa kwa uratibu wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa kwa serikali kuhusu harakati za uchaguzi, kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa, tume huru ya uchaguzi.”

Kuhusu kukabiliana na ukwepaji sheria, amesema kuwa bado kumeenea dhana ya sheria inayoegemea upande mmoja miongoni mwa raia wa Côte d’Ivoire, ingawa uchunguzi unafanyika sasa kuhusu vitendo vya uhalifu mkubwa uliotendwa wakati wa uchaguzi wa 2010/2011.

“Natoa wito kwa serikali ya Côte d’Ivoire kuendelea na uchunguzi wake ili kuwafikisha mbele ya sheria wale wanaodaiwa kukiuka haki za binadamu, kwani haki, bila kupendelea egemeo la kisiasa, inaweza kuchangia sana kuponya vidonda vya zamani na kuimarisha maridhiano.”

Kuhusu sekta ya usalama, amesema serikali imejitahidi katika kushughulikia malalamishi makubwa kufuatia maandamano ya Novemba 2014 ya baadhi ya wanajeshi, kwa kujenga kambi za jeshi na kulipa mishahara, na pia kupitisha sheria kuhusu utaratibu wa jeshi la taifa.