Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shinikizo linazidi Ugiriki, wahamiaji 600 wakiwasili kila siku

Shinikizo linazidi Ugiriki, wahamiaji 600 wakiwasili kila siku

Nchini Ugiriki, wakimbizi na wahamiaji wanazidi kuwasili kwenye kisiwa cha Lesvos kilichopo katikati mwa bahari ya Mediteranea, huku uwezo wa kuwapokea ukizidiwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR, watu 600, hasa kutoka Syria, Afghanistan na Iraq wanawasili kila siku kwenye visiwa vya Ugiriki kwa njia ya boti za plastiki au mbao, idadi yao ikiwa imeongezeka sana tangu mwanzo wa mwaka huu.

Msemaji wa UNHCR Adrian Edwards amewaambia leo waandishi wa habari mjini Geneva kuwa idadi ya wakimbizi hao imefika 7,200 mwezi Mei, wakati ilikuwa 737 tu mwezi Januari.

Amesema mamia ya wahamiaji wanasafirishwa kila siku kwenda Ugiriki bara baada ya kusajiliwa, lakini bado zaidi ya watu 2,000 wamepewa hifadhi kwenye vituo mbalimbali kisiwani humo, huku nafasi ya kuwapokea ikizidiwa maradufu na zaidi .

"Mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali tunayoshirikiana nayo yanatoa huduma za dharura kwenye kijiji cha Moria, ikiwemo kufuatilia watoto wasiosindikizwa na mtu yeyote, pia huduma za afya na kisaikolojia. Idara ya mapokezi ya wizara ya mambo ya ndani inawajibika kwa kusajili watu wanaowasili. UNHCR inaongeza shughuli zake nchini Ugiriki na Italia kusini kutokana na ongezeko kubwa la wahamiaji na wakimbizi wanaowasili"