Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi hatarini kutumbukia machafuko zaidi- Kamishna Zeid

Burundi hatarini kutumbukia machafuko zaidi- Kamishna Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ameeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa vitendo vya machafuko na vitisho kutoka kwa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Burundi, akisema kuwa vitendo hivyo huenda vikaifanya hali ambayo tayari ni tete kuzorota zaidi. Taarifa kamili na Joshua Mmali

Kamishna Zeid ametoa wito kwa mamlaka za Burundi kuchukua hatua za dhati kuwadhibiti wanamgambo hao na vitendo vyao.

Amesema kila siku, Ofisi ya Haki za binadamu hupokea simu 40 hadi 50 kutoka kwa watu wenye hofu kubwa kote nchini, wakiomba ulinzi au kuripoti dhuluma. Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi ya haki za bindamau, Geneva

"Tumepokea pia maelezo kutoka kwa wakimbizi waliokimbilia nchi jirani kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoripotiwa kufanywa na wanamgambo wanaounga mkono serikali, wakijulikana kama Imbonerakure. Uhalifu huo unadaiwa kufanyika Bujumbura na katika mikoa mingine, ukiwemo mauaji, utekaji nyara, utesaji, vipigo na vitisho vya kifo na aina nyingine za unyanyasaji."

Bwana Colville amesema taarifa hizo ni kutoka kwa wakimbizi 47 waliohojiwa na maafisa wa haki za bindamu katika kambi za wakimbizi nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.