Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashauriano kuhusu Yemen kuanza Juni 14 Geneva

Mashauriano kuhusu Yemen kuanza Juni 14 Geneva

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha utayari wa Rais Abd Rabou Mansour Hadi wa Yemen wa kutuma ujumeb wake kushiriki kwenye mashauriano kuhusu mustakhbali wa amani nchini mwake.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema utayari huo umenukuliwa kutoka kwa mjumbe maalum wa Katibu Mkuu kwa Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed kutoka Riyadh na mashauriano hayo yamepangwa kuanza Geneva, Uswisi tarehe 14 mwezi huu.

Bwana Ban amesisitiza wito wake wa dharura kwa pande zote nchini Yemen kushiriki kwa dhati na kwa nia njema kwenye mashauriano hayo bila masharti yote kwa maslahi ya wananchi wote.

Amesisitiza uzingatiaji wa maazimio ya baraza la usalama yanayolenga kuhakikisha mashauriano hayo yanakuwa shirikishi  na jumuishi na kila pande ziweke mazingira bora ya kisiasa ili yaweze kufanikiwa.

Halikadhalika amerejelea wito wake wa sitisho jingine la mapigano ili kuwezesha misaada ya kibinadamu kufikia wahitaji nchini Yemen, akisema hali hiyo inaweza kuweka mazingira bora zaidi ya mashauriano ya amani.