Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Afghanistan unasababisha vifo vya maelfu ya watu- UM

Mzozo wa Afghanistan unasababisha vifo vya maelfu ya watu- UM

Mzozo unaoendelea nchini Afghanistan unasababisha maelfu ya watu kuuawa au kujeruhiwa, na kulazimu familia nyingi kukimbia makwao, amesema Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Afghanistan, Mark Bowden.

Bwana Bowden amesema, kufikia Aprili 30, raia wa Afghanistan 1,989 walikuwa wamejeruhiwa kutokana na mzozo huo, huku 978 wakiwa wameuawa kote nchini.

Ameongeza kuwa idadi ya majeruhi katika hospitali ya dharura ya Kabul inadhihirisha athari mbaya mno za mzozo huo, akisema madaktari kwenye hospitali hiyo wamemweleza kuwa kumekuwa na ongezeko la asilimia 50 kwa idadi ya raia waliojeruhiwa mwaka huu, ikilinganishwa na wakati kama huu mwaka uliopita.

Akizungumza wakati wa jukwaa la wanahabari na wawakilishi wa kijamii mjini Kabul, Bwana Bowden ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Afghanistan, UNAMA, amesema kuchacha kwa mapigano mwaka 2015 kumeongeza shinikizo kwa uwezo wa kutoa usaidizi wa kibinadamu.