Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kijamii ni muhimu katika kutatua mzozo wa Syria- de Mistura

Mashirika ya kijamii ni muhimu katika kutatua mzozo wa Syria- de Mistura

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura, amesema leo kuwa mashirika ya kijamii yanaweza kuchangia pakubwa katika kutatua mzozo wa Syria, hususan kupitia juhudi za kuhakikisha kuwa maoni na matakwa ya sehemu zote za jamii yanazingatiwa, na kwa kuwakilisha sauti za watu mashinani.

Bwana de Mistura, ambaye anaendelea kufanya mashauriano na wadau mbali mbali, wakiwemo Wasyria na wawakilishi wa kikanda na kimataifa, amesema kuwa mchango wa mashirika ya kijamii ni muhimu katika kutafuta suluhu endelevu la kisiasa, ambalo litaendeleza haki za binadamu, ujumuishaji wa maoni ya wengi na demokrasia.

Bwana de Mistura amesema hayo alipokutana leo na ujumbe wa Wakfu wa Aga Khan, ukijumuisha Mabwana Mohammad Wardeh, Mohammad Seifo na Ali Esmaiel, ambapo wamejadili hali ilivyo na kubadilishana mawazo kuhusu kutafuta suluhu la kisiasa, na hususan jinsi ya kutekeleza makubaliano ya Geneva yaliyopitishwa na kundi la kuchukua hatua.