Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yataka mabadiliko kuhusu uzalishaji wa chakula

FAO yataka mabadiliko kuhusu uzalishaji wa chakula

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO, Jose Graziano da Silva, ametoa wito wa uwiano kati ya chakula, kilimo na mazingira katika ujumbe wake wa Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 5.

Bwana Da Silva amesema kwamba wananchi, wazalishaji na wawekezaji ni muhimu wapate mtazamo mpya kifikra na kivitendo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwa ajili ya kulisha idadi inayoongezeka ya watu

Akizungumza katika maonyesho ya Milan, EXPO 2015 Da Silva ametaja mambo mawili ikiwemo, kuhakikisha kwamba kila mtu ana chakula  na kwamba mifumo ya chakula ni endelevu kwani ni muhimu kuhakikisha  kuna juhudi mahsusi kwa ajili ya kulisha ulimwengu mzima huku rutuba ya udongo na raslimali nyinginezo zikilindwa.

Aidha amesema mabadiliko ya tabianchi yanahatarisha uhakika wa chakula kwa siku zijazo hususan kwa ajili ya athari zake kwa uzalishaji wa bidhaa za kilimo katika mataifa maskini yanayoendelea na inatishia uwepo wa mataifa ya visiwani.