UNHCR yasikitishwa na utekaji nyara wa raia wa Eritrea

UNHCR yasikitishwa na utekaji nyara wa raia wa Eritrea

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR) limesema, linawasiwasi mkubwa na taarifa ya hivi karibuni ya kutekwa nyara kwa raia 14 wa Eritrea ambao ni waomba hifadhi mashariki mwa Sudan Alhamisi juma hili .

Tukio hilo lilitokea wakati kikundi cha waasi kwenye lori lilipoanza kupiga risasi msafara ulioandaliwa na Shirika la Sudan la Kuhudumia Wakimbizi (COR), ambao ulikuwa unasafirisha waeritrea 49 waomba hifadhi kutoka kituo cha mapokezi cha Wad Sharifey karibu na Kassala wakielekea kambi ya wakimbizi ya Shagarab.

Waomba hifadhi 14 waliotekwa nyara ni pamoja na watoto saba bila ya wazazi wao kati yao wavulana sita na msichana mmoja, wanawake watano na wanaume wawili. Aidha, waomba hifadhi sita walipata majeraha madogo waliporuka kutoka kwenye gari hilo.

UNHCR inatoa msaada kwa manusura, ambao wamehamishiwa katika kambi ya Shagarab na wanashirikiana na mamlaka ya Sudan ambao wanachunguza tuhuma hizo . UNHCR inakaribisha uchunguzi huo na imeiomba serikali kufanya kila liwezalo na kuwaleta mbele ya sheria wahusika. UNHCR inataka safari za waomba hifadhi zifuate utaratibu maalum na kusindikizwa na vikosi vya usalama.

Kabla ya tukio hilo, Serikali ya Sudan na UNHCR wameshuhudia kupungua kwa utekaji nyara na biashara haramu katika eneo la mashariki kutokana na ushirikiano wa kupambana na suala hili unaoendelea baina ya UNHCR na serikali. Katika siku za nyuma, serikali ilitoa dhamira ya kupambana na jambo hili na kupitisha mkakati wa 2015-2017 wa kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, magendo na utekaji nyara nchini Sudan.