Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumaini yaanza kuibuka Ukraine: Baraza la Usalama

Matumaini yaanza kuibuka Ukraine: Baraza la Usalama

Licha ya mapigano yanayoendelea mashariki mwa Ukraine, kuna matumaini ya kumalizika kwa mgogoro amesema leo Jeffrey Feltman, mkuu wa Idara ya maswala ya kisiasa ya Umoja wa Mataifa, akihutubia Baraza la Usalama kuhusu Ukraine.

Bwana Feltman amesema mapigano na ghasia vimeanza kupungua tangu kusainiwa kwa makubaliano ya Minsk ya tarehe 12 Februari, halikadhalika, idadi ya vifo na majeraha.

Amepongeza jitihada za kidiplomasia ya Ukraine, Ufaransa, Ugerumani na Ufaransa katika kufikisha makubaliano hayo.

Aidha amesikitishwa na baadhi ya ukiukwaji wa sitisho la mapigano unaoendelea kushuhudiwa, ikiwemo kurushwa kwa makombora kila siku, kutega mabomu ardhini au kuwepo kwa askari wa kigeni nchini Ukraine.

Kwa upande wa kibinadamu, Bwana Feltman amesema hali bado ni tete idadi ya wakimbizi ikiwa imefika zaidi ya milioni 1.3.

(SAUTI FELTMAN)

«  Idadi ya wakimbizi wa ndani  itaendelea kuongezeka iwapo ghasia itaendelea. Wasiwasi wetu mkubwa pia ni kushindwa kufikisha misaada ya kibinadamu kwa  watu waliopo katikati ya mapigano, kwa sababu za kibinadamu.  Hatua hii huzuia msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha kwa wanaohitaji zaidi. Pande zote za mzozo zinapaswa kuhakikisha mara moja kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na Mashirika yasiyo ya kiserikali wanaweza kufikisha misaada ya kibinadamu bila kizuizi chochote »