Uchunguzi zaidi ufanyike kuhusu watu waliolazimika kutoweka CAR- UM

5 Juni 2015

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, imezitaka serikali za Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na Jamhuri ya Kongo zifanye uchunguzi ili kuwawajibisha askari wa vikosi vya kigeni waliotenda uhalifu katika CAR mnamo mwaka 2014.

Ikitaja aina moja ya uhalifu huo, Ofisi hiyo imeeleza kusikitishwa kwamba, zaidi ya miezi 15 tangu vikosi vya wanajeshi kutoka Jamhuri ya Kongo kuwalazimu watu wapatao kumi na mmoja kutoweka, bado hatma ya watu hao haijulikani, huku uchunguzi wa kina ukiwa bado haujafanywa na mamlaka husika ndani au nje ya nchi.

Kulingana na ushahidi uliotolewa na watu kadhaa waliohojiwa na wafanyakazi wa ofisi hiyo ya haki za binadamu, watu 11 walikamatwa katika mji wa Boali ulioko takriban kilomita 80 kaskazini mwa Bangui, na kuzuiliwa baada ya ufyatulianaji risasi kati ya anti-Balaka na wanajeshi wa Jamhuri ya Kongo waliokuwa chini ya vikosi vya Muungano wa Afrika, MISCA.

Ripoti zinadai kuwa wanajeshi hao wa MISCA wametenda vitendo vya kulazimisha watu kutoweka, utesaji na mauaji ya kiholela.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter