Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid ataka waliokiuka haki Nigeria wakabiliwe kisheria

Zeid ataka waliokiuka haki Nigeria wakabiliwe kisheria

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ametoa wito wa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria wale wote waliokiuka haki za binadamu Nigeria.Taarifa kamili na Amina Hassan.

(Taarifa Amina)

Kamishna Zeid amesema mahojiano na watu waliokimbia au kunusuriwa kutoka miji iliyokuwa imetekwa na Boko Haram, yameweka picha ya unyama na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliotekelezwa na waasi hao wa kigaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Amesema mahojiano hayo pia yamebainisha madai ya ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu na ile ya kibinadamu, ukidaiwa kutekelezwa na wanajeshi wa serikali ya Nigeria.Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi ya haki za binadamu mjini Geneva.

"Mmoja wa wahanga ambaye alishukiwa kuwa Boko Haram alitueleza yalioyomkumba baada ya kukamatwa na kuzuiliwa Yola na wanajeshi katika jimbio la Adamawa, mwanamume huyo alisema alikaa siku tano bila majia au chakula huku akisema kwamba kulikuwa na wastani wa vifo tano kila siku kizuizini.Tangu hapo tumeendelea kupata ripoti za kukamatwa kiholela, mateso na mauaji ya halaiki na ukosefu wa ulinzi wa raia wakati wa operesheni za kusaka wahalifu.Tunatambua changamoto inayokabili serikali ya Nigeria na serikali zingine katika ukanda wakati wa kukabiliana na Boko Haram lakini ni muhimu waheshimu sheria kulingana na wajibu wao wa haki za kibinadamu."

Kamishna Zeid amesema raia kaskazini mashariki mwa Nigeria wamekuwa wakishuhudia unyama na ukatili wa kutisha unaofanywa na Boko Haram. Ametaja vitendo vya mauaji kiholela, kutumikishwa kwa lazima katika jeshi, ukiwemo kuwatumia watoto kulipua mabomu, katika ajira za lazima, ndoa za lazima, ukatili wa kingono na ubakaji.