Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA yamchunguza askari wake kwa madai ya uhalifu wa kingono

MINUSCA yamchunguza askari wake kwa madai ya uhalifu wa kingono

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, MINUSCA, umetangaza leo kuwa umepokea taarifa za madai ya ukatili wa kingono dhidi ya mtoto, yakimhusisha mmoja wa askari walinda amani mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric, amesema kuwa Mkuu wa ujumbe huo, Babacar Gaye alianzisha uchunguzi mara moja baada ya kupokea taarifa hizo, na kujulisha mamlaka za CAR.

Amekariri kuwa kulingana na sera ya Umoja wa Mataifa ya kupinga kabisa uhalifu wa kingono, hatua zimechukuliwa za kumlinda mwathiriwa, ambaye pia amehudumiwa ipasavyo. Umoja wa Mataifa pia umeiomba serikali anakotoka askari huyo kuanzisha uchunguzi mara moja.”

Hiki si kisa cha kwanza cha madai ya ukatili wa kingono unaodaiwa kufanywa na walinda amani dhidi ya watoto nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Tayari uchunguzi unaendelea kuhusu madai ya askari wa Ufaransa kuwanyanyasa watoto kingoni nchini humo.